Habari

MWAKYEMBE ATOA SALAMU ZA POLE KWA MSIBA WA LIMONGA JUSTINE… watoto wake kulipiwa ada na vifaa vya shule, Radio Uhuru yasema pengo lake ni kubwa

on

WAZIRI wa Habari Utamaduni na
Michezo, Dk. Harryson Mwakyembe ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu
Limonga Justine aliyejiwekea jina kubwa kwa jamii na amewaomba wafiwa kuwa na
subira katika kipindi hiki kigumu cha simanzi na majonzi.
Amesema, anatambua ukubwa wa msiba huu hasa katika nyanja ya habari, lakini hata hivyo hakuna budi kuwa na uvumilivu na kumuombea Mungu marehemu apokelewe mahala pema. 
Naye bosi wa Nduvini Auto Garage ya
jijini Dar es Salaam, Alhaji Ahmed Msangi ameonyesha kuguswa na tukio la msiba
wa aliyekuwa mtangazaji wa Uhuru Fm, Limonga Justine aliyemwelezea kuwa ni
miongoni mwa wanahabari waliotoa mwongozo wa kuigwa kwenye jamii.
Msangi amesema kuwa, alimfahamu
vyema Limonga na kwamba alipopokea taarifa za kifo chake alihisi kuishiwa nguvu
kutokana na ukaribu waliokuwa nao.
Bosi huyo ameahidi kuwa katika
kipindi hiki cha kufunguliwa kwa shule, kampuni yake itawanunulia watoto wa marehemu
vifaa vya shule zikiwemo sare pamoja na kuwalipia karo wakati wakisubiri kukaa
na familia kuona namna ya kuwazesha watoto hao kielimu.
Wakati huohuo, kaimu mkurugenzi
wa Uhuru Fm, Angel Akilimali amesema kifo cha Limonga aliyekuwa mwajiriwa wao
kimeacha pengo kubwa ambalo halitazibika kirahisi.
Alisema Limonga alikuwa mhariri
mbunifu aliyeweza kuongoza vipindi mbalimbali ambavyo vilipendwa na
wasikilizaji wao. Angel ameahidi kuwa, stahiki zote za marehemu kama mwajiriwa
zitapatikana kwa wakati.
Limonga amefariki dunia Desemba 30, mwaka jana katika hospitali ya TMJ alikolazwa akitibiwa. Ameacha mjane na watoto wawili ambapo mazishi yake yamefanyika leo katika makaburi ya Saku, Mbagala Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *