Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: PAPII KOCHA MSAHAU KWAO MTUMWA

on

Onyesho la mtu na baba yake (Papii Kocha na Nguza Vicking) lililofanyika Jumamosi iliyopita katika ukumbi wa King Solomon, linaashiria mapungufu kadhaa ya kiufundi kwa Papii na timu yake iliyomzunguka.

Sina tatizo kabisa na mzee wangu Nguza Vicking, kwangu mimi huyu ni mtunzi mzuri na mmoja wa wapiga magitaa mahiri sana kuwahi kutokea nchi hii, lakini kamwe sikuwahi kuamini kuwa ni mwimbaji mzuri.

Nguza alisimama vema kwenye nafasi yake kama mpiga gitaa, lakini hakuwafurahisha mashabiki waliokwenda kufuata sauti yake. Hili si kosa lake, ni kosa la mashabiki hao kutojua Nguza ni mahiri katika upande upi.

Show ya Vicking’s Night ilikaa ki-bongo fleva zaidi pengine ni kwaajili ya kufuata upepo wa biashara maana muziki wetu wa dansi unahitaji maombi, lakini pamoja na hayo, ni mirindimo na vionjo vya dansi ndivyo vingeweza kuusisimua ukumbi.

Taratibu namuona Papii akielemea kwenye muziki wa bongo fleva, muziki ambao show zake hubebwa zaidi na ujumbe na melody kuliko namna ya utumbuizaji.

Sijambo baya kwa Papii kuegemea bongo fleva lakini ni vema akakumbuka alikotoka, akakumbuka kile kilichomfanya awe staa, kile kilichomfanya awe Papii Kocha.

Papii aliibuka kama rapa wa muziki wa dansi, sauti yake tamu ikapenya kwenye masebene ya bendi za FM Academia na Beta Musica, baadae akaanza kuonyesha pia umahiri wake kwenye uimbaji. Hata Pale TOT Plus alipokaa kwa muda mfupi aliacha sifa kubwa sana kupitia rap na uimbaji wake.

Papii alikuwa mkali wa kushambulia jukwaa, fundi wa kuteka hisia za mashabiki kupitia rap zake nyingi ikiwemo ile “Nehi nehi babujii” ambayo ilikuwa gumzo kila kona.

Kwa mtazamo wangu (si lazima niwe sahihi) Papii alipaswa kuandaa kitu japo cha dakika tano ambacho kingeuzibua ukumbi kwa mayowe.

Angeweza kutengeneza show fupi ya ufunguzi ambayo ingekuwa ya sebene kali, akaibuka ukumbini na madansa wake, akashambulia jukwaa huku akiminina rap zake zilizopata umaarufu. Hapo angekuwa amemaliza kila kitu.

Baada ya hapo angeendelea na nyimbo zake za pole pole na waimbaji wake walipooza, hakuna ambaye angemlaumu na wala asingeibuka msanii mwingine wa kuiteka show kama alivyofanya Q Chillah. Kwenye show ya Aslay na Nandy pale Escape One, Papii alikuwa huyu huyu aliyepooza, lakini sikujali, nilijua anaficha makucha yake  kwa kuwa pale alikuwa mwalikwa tu.

Zamani watu walikuwa wanakwenda Diamond Jubilee kuangalia uzinduzi wa albam za bendi kama Twanga Pepeta na nyinginezo kwaajili ya kuona tu bendi inaingia vipi jukwaani na staa wa bendi anaingia vipi, baada ya hapo robo ya watu huondoka ukumbini. Kiu yao ilikuwa ni hiyo tu.

Papii anapaswa kufahamu kuwa kitu cha kwanza (first impression) unachokifanya jukwaani ndiyo chenye nafasi nzuri ya kuacha kumbukumbu kubwa kwenye akili ya mtu.  Hapa dawa ilikuwa ni kufungua show yake na moto mkali wa sebene, watu wangeshika adabu yao.

Papii akumbuke ahadi aliyoitoa wakati ametoka jela kwa msamaha wa Rais – kwamba wanakuja kuukomboa muziki wa dansi, ajue kuwa watu wengi wanamtegemea katika hilo hivyo asisahau kule alikotoka na kujivika usasa ambayo utapoteza kabisa utambulisho (identity) wake.

Achukue mazuri ya bongo fleva, mazuri ya dansi na kisha afanyie kazi mapungufu ya muziki wa dansi kisha apenye katikati na kuibuka ladha ya kipekee kama alivyofanya Christian Bella. Lakini kubwa kuliko yote atambue kuwa mashabiki wake hawajamzoea Papii aliyepooza jukwaani.

Mimi binafsi hata wimbo wake wa “Waambie” nauona wa kawaida sana ingawa ni wimbo sahihi kuingia nao sokoni baada ya janga lililomkuta la kukaa jela kwa miaka 13. Naamini kuwa nyimbo za ukweli kutoka kwa Papii ziko njiani.

Comments

comments

About Saluti 5

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *